Dar – Maelezo

Kongamano la CHAUKIDU 2017 Dar es Salaam

Dira ya Karne ya 21– Ukuaji wa Kiswahili na Ustawi wa Jamii ya Wazungumzaji wake

 

Ni suala lisilohitaji mjadala kwamba lugha ya Kiswahili, kama zilivyo lugha zote duniani, iliinukia, ikakua, na inaendelea kukua katika maana halisi ya neno ‘kua’ – “kitendo cha kuongezeka kimo, ukubwa au uwezo” (Kamusi la Kiswahili Fasaha – BAKIZA, 2010). Kwa hakika, mjadala kuhusu ukuaji wa Kiswahili umetendewa haki stahiki na wanazuoni katika taaluma za isimu, isimujamii, na fasihi ya Kiswahili. Matokeo ya tafiti anuai kuhusu historia na maendeleo ya Kiswahili yamechapishwa katika majarida na vitabu mbalimbali. Taarifa na mijadala katika machapisho haya inathibitisha jambo moja muhimu kwamba lugha ya Kiswahili na matumizi yake yamekuwa yakipanuka tena kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na msamiati na istilahi zake kuongezeka, nyanja za matumizi yake kupanuka, idadi ya watumiaji na wazungumzaji wake kuongezeka, hadhi na dhima yake kupaa juu, nk. Mintaarafu ya ukweli huu, kunatuelekeza kudai kuwa kukua kwa Kiswahili ni ushahidi kuntu wa kukua na kustawi kwa jamii ya wazungumzaji wa Kiswahili hususan katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati ambako hapana shaka ndiko lugha hii ilikoinukia.

Lugha isiyotumika au kutumiwa huvia na hatimaye hutoweka/hufa. Lugha inayotumiwa hukua na kustawi kulingana na mahitaji ya mawasiliano yaliyomo katika jamii husika. Mawasiliano ya lugha huwa nyenzo kuu katika kufanikisha shughuli za binadamu – iwe ni za kiuchumi au kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kifasihi, huduma za kiroho, kiteknolojia na kisayansi, kielimu, nk. Katika mchakato wa kukidhi mahitaji ya mawasiliano hayo, msamiati na istilahi zake hupanuka, aina mbalimbali za uzungumzaji na matumizi yake huchipuka, huchochea ubunifu katika tasnia anuwai kama vile katika sanaa za lugha na maonesho, uvumbuzi na ugunduzi wa kisayansi na kiteknolojia, utawala na siasa, usalama na ulinzi, uzalishaji, afya bora, elimu bora, nk. Hivyo basi, vilevile, ustawi wa jamii huweza kuakisi na kusawiri ukuaji wa lugha husika.

Kongamano la tatu la kimataifa la CHAUKIDU litakalofanyika jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania linalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa Kiswahili duniani kote kujadili mchango wa kila tasnia), uwanja wa maarifa eneo la kijiografia eneo la kijamii (matabaka, marika, jinsia, nk), lahaja, nk katika kukiendeleza na kukinawirisha Kiswahili. Kongamano litajadili jinsi kila tasnia ilivyochangia na inavyoendelea kuchangia kwa namna tofautitofauti katika kukuza Kiswahili na/au vivyo hivyo jinsi ambavyo Kiswahili kilichangia na kinaendelea kuchangia kustawisha eneo au tasnia husika. Inatarajiwa kwamba mawasilisho, mazungumzo, na mijadala itakuwa chimbuko ama kichocheo cha kuanza kutafakari juu ya uundaji wa DIRA ya ukuzaji endelevu wa Kiswahili na ustawi endelevu wa jamii katika karne ya 21 na hata miaka Alfu Lela Ulela!

Kwa hivyo basi, Kongamano hili ni fursa kwa wapenzi wa  Kiswahili, walimu, wanafunzi, watafiti, waandishi, wanahabari, wanasiasa, wasanii, wakuzaji wa mitaala, , maafisa wa lugha, wachapishaji, wanasayansi, wanaTEHAMA, wafanyabiashara, n.k., kubadilishana na kuelimishana kuhusu maarifa, weledi, tajiriba, taaluma, n.k.