CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Director

Filipo Lubua, PhD
Chaukidu Director
University of Pittsburgh
lubua@pitt.edu 

Ndugu WanaCHAUKIDU na wapenda Kiswahili kote duniani,

Ninayo furaha kubwa sana kuchaguliwa Mkurugenzi wa chama hiki kikubwa cha wapenda Kiswahili duniani.  Baada ya kuona kazi kubwa iliyofanywa na bodi zote zilizotangulia, nitajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mafanikio yote yaliyokwisha kupatikana. Nitahitaji ushirikiano mkubwa toka kwa Bodi na wanachama wote kwa ujumla.

Tangu kuanzishwa kwake, CHAUKIDU kimejipambanua dhahiri shahiri kuwa ni chama cha kidunia, ambacho kina lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa Kiswahili wakiwemo wanadayaspora, waalimu na wakufunzi, watafiti, wanaisimu, wanahabari, wafanyabiashara, watoa huduma za utalii, watunga sheria za lugha, wasanii, na wazungumzaji wa Kiswahili kwa ujumla. Kwa miaka kadhaa sasa tangu CHAUKIDU kianzishwe rasmi mwaka 2011 na kuzinduliwa rasmi jijini Washington DC mwaka 2015 na Rais Ali Hassan Mwinyi, tumeweza kupata ufuasi toka kwa watu wengi na taasisi nyingi. Tumeweza kushirikiana na watu na taasisi mbalimbali kueneza agenda yetu ya umajumui wa wazungumzaji na warithi wa Kiswahili waliosambaratika kila pembe ya dunia, pasipo kujali nchi zao za asili au uraia wao.

Japo tumeweza kupata wafuasi wengi, bado idadi kubwa ya wafuasi hawa wamekuwa ni wadau wa taaluma za Kiswahili walioko katika vyuo mbalimbali, hasa walimu wa Kiswahili wafundishao katika vyuo vilivyoko katika dayaspora na wale wafundishao katika vyuo vilivyoko Afrika Mashariki. Ingawa hata hili ni jambo kubwa la kujivunia, bado tuna kazi kubwa zaidi ya kuwaleta wadau wenzetu wengi walioko katika tasnia nyingine zitumiazo Kiswahili. Wakati ambapo mwamko wa kukitambua Kiswahili kama lugha ya majivuni na lugha ya kuwaunganisha Waafrika na wote wenye asili ya Afrika umekuwa mkubwa sana, ni vyema tukajitahidi kufanya harakati za kiuenezi ili kuwapata wafuasi wengi zaidi wa kada zote za kijamii.

Katika Bodi hii ya awamu ya nne, pamoja na mambo mengine mengi, nitajitahidi kupambania malengo makuu manne: kwanza kuongeza ufuasi kwa watu wasio wa kada ya ualimu na ukufunzi na wasio miongoni mwa wanataaluma za Kiswahili. Pili, kuitambulisha zaidi jumuiya ya CHAUKIDU kwa viongozi wa kiserikali na wa jumuiya za kikanda katika maeneo yote Kiswahili kizungumzwapo. Tatu, kushiriki katika shughuli, harakati, na mikakati ya kijamii ili kuifikia jamii yetu katika namna dhahiri na ya kiuhalisia zaidi. Nne, kutambua mchango wa wale ambao wamefanya kazi kubwa na ya kipekee katika uenezi wa Kiswahili kwa ajili ya kuwatia shime wengine waendeleze juhudi hizo. Kuyafikia yote haya, ni sharti kuendeleza mikutano na makongamano ya Kimataifa ya Chaukidu yatakayofanyika katika nchi mbalimbali ili kuleta hamasa zaidi kwa wanachama walioko katika maeneo hayo. Ni sharti makongamano haya tuyaboreshe zaidi ili yaweze kuvutia wa kila aina.

Tunakuhitaji uungane nasi ili tuweze kuyafikia malengo yetu. Ikiwa bado hujawa mwanachama, tafadhali njoo tuungane. Kama nilivyoeleza hapo mwanzoni, chama hiki ni cha kila mtu, bila kujali ni wa kada au tasnia gani; bila kujali ni mzaliwa au raia wa nchi gani. Ni chama cha kuwaleta Waswahili na wadau wa Kiswahili pamoja. Tafadhali njoo ujiunge nasi. Vilevile, tutafurahia kupata maoni na ushauri toka kwa mtu yeyote wa mahali popote. Kwa ushauri na maswali, usisite kuniandikia barua pepe kupitia anuani-pepe ya chama: chaukidu@gmail.com au anuani-pepe yangu binafsi: lubua@pitt.edu.