Maelezo Nairobi 2016

Kongamano la Chaukidu 2016 Nairobi

Taaluma za Kiswahili Karne ya 21 Nyumbani na Ughaibuni: Tutokako, Tulipo, na Tuendako

Kiswahili sio tu lugha ya Kiafrika izungumzwayo na wazungumzaji wengi kuliko lugha nyingine yo yote ya Kiafrika barani Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, bali pia ndiyo lugha ya Kiafrika inayoongoza kwa kuwavutia wanafunzi wengi wa kigeni katika vyuo vikuu ughaibuni na kuonekana kama ‘uti wa mgongo’ wa programu yo yote ile inayojiita programu ya lugha za Kiafrika katika vyuo vikuu vingi duniani. Nchini Marekani takriban vyuo vikuu mia moja vinafundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni, shughuli iliyoanza mwanzoni mwa miaka ya 1960, na hapana shaka imekuwa endelevu. Swali ambalo linaibua haja ya mjadala ni iwapo kuna uhusiano wowote kati ya uhai na ustawi wa lugha nyumbani na ustawi wake ughaibuni?

Kiswahili kimestawi na kurutubishwa na virutubishi vya aina mbalimbali na ambavyo vimekuwa vikibadilika kutoka zama moja hadi zama nyingine. Zama za zama Kiswahili kilizungumzwa na makundi mbalimbali ya wenyeji katika ukanda wa pwani ya Afrika ya Mashariki na visiwa vya mwambao huo. Wakati Wamishenari wa Kikristo wakiwasili Afrika ya Mashariki katika miaka ya katikati ya karne ya 19, Kiswahili kilikuwa kimeshaenea barani kutokana na athari za ukoloni na mwingiliano wa utawala wa Kiarabu na utamaduni wa Waafrika wa mwambao huu. Wamishenari na wakoloni wa Kizungu walikienyejisha Kiswahili kama mojawapo ya lugha kuu za kufundishia dini ya Kikristo na kufundishia shuleni. Ujio wa watawala wa kikoloni mwishoni mwa karne ya 19 na ustawi wa utawala huo katika nusu ya kwanza ya karne ya 20 ulishuhudia ukuaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika utawala hususan ngazi za chini.

Maendeleo ya Kiswahili yalipiga hatua mpya mnamo mwaka wa 1930 serikali ya kikoloni ya Waingereza ilipounda Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki na kupewa jukumu la kusanifisha lugha ya Kiswahili ili kuwa na lugha moja “sanifu” kutoka kwa lahaja nyingi za Kiswahili zinazozungumzwa upwa wa Afrika Mashariki. Kamati hii ndiyo iliyokuwa na kuibuka kuwa Chuo Cha Kiswahili, baadaye kufanywa sehemu ya taaluma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kubatizwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Hii leo, asasi hii imekuzwa kuwa mojawapo ya vitivo muhimu na maarufu vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinachojulikana kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).

Katika kipindi cha ukoloni, Kiswahili hakikuishia kuwa lugha ya kuwezesha utawala wa kikoloni tu, bali pia kilijitokeza kuwa lugha ya kuwezesha harakati za wananchi wa Afrika ya Mashariki za kudai uhuru. Hatimaye, baada ya uhuru kupatikana katika miaka ya sitini, Kiswahili kiliendelea kuwa lugha ya taifa, isitoshe kilitumika kama lugha ya utawala, biashara, siasa, habari, kufundishia shuleni, somo la shuleni na taaluma katika vyuo. Leo hii si rahisi kupata chuo nyumbani kisichokuwa na idara ya Kiswahili. Nje ya Afrika Mashariki, Kiswahili hivi leo kimepata mashiko kama mojawapo ya somo la msingi linalofundishwa na idara za lugha za kigeni za vyuo vikuu vingi vitajika vya Ulaya na Marekani Kaskazini.

Mintaarafu usuli huu, mkutano huu unalenga kuwa uwanja wa kukutanisha wadau wa aina zote wa Kiswahili walio nyumbani na ughaibuni kutafakari na kujadili mwelekeo na mustakabali wa lugha ya Kiswahili katika karne ya 21 na baadaye. Kongamano hili linalenga kuwapa nafasi walimu, wanafunzi, watafiti, waandishi, wanahabari, wanasiasa, wasanii, watengenezaji mitaala, wanautamaduni, maafisa wa lugha, wachapishaji, n.k., kwa kuzingatia mtiririko wa maarifa, weledi, tajriba, taaluma, n.k. kati ya nyumbani na ughaibuni.