Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) chaukidu@gmail.com

Mussa M. Hans, Ph.D.
Mkurugenzi wa CHAUKIDU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Ndugu msomaji, mpenzi wa Kiswahili, mgeni, mkereketwa, na mdau unayeitembelea tovuti hii kwa mara ya kwanza au kwa mara nyingine, ninakukaribisha kwa moyo mkunjufu. Nina furaha kuwa Mkurugenzi wa CHAUKIDU wa awamu hii ya tano. Ni heshima kubwa kupewa fursa ya kukuhudumia wewe binafsi na jumuiya yetu pana. Hakuna fursa adhimu kama ya kuwahudumia watu wanaojali na kukipenda kinachojengwa. Kiswahili ni lugha ya wengi na tafiti nyingi zinaonesha lugha ni kitambulisho – kuna tija itokanayo na mshikamano na ushirikiano wa wahusika. Tungependa CHAUKIDU kitambulikane kwa ubora wa huduma yake kwa jamii.

Katika awamu hii, lengo letu kubwa ni kuyaona maendeleo ya Kiswahili yakidhihirika katika jamii zetu. Kwa bahati nzuri tunachukua hatamu za uongozi wakati mzuri sana kihistoria ambapo Kiswahili kinapigiwa debe kote barani Afrika kwa nia njema. Iwe lugha itakayofundishwa shuleni na vyuoni kama lugha ya Afrika. Jambo hili ni muhimu na ni fursa kubwa na ya kipekee. CHAUKIDU kama chama kinaazimia kuwa mstari wa mbele katika masiala haya kwa kutoa ushauri, utaalamu na mafunzo yatakayowafaa wengi ambao watawania fursa za kukifundisha Kiswahili sehemu mbalimbali za Afrika na dunia nzima. Nia ni kuwa na walimu na mabalozi wanaoelewa sayansi ya kufundisha lugha kwa wageni. Nyingi za nchi zinatambua umoja na haja ya kufanya mambo pamoja. CHAUKIDU kinaipigia debe lugha ya Kiswahili ili iwe lugha ya Afrika, lugha asili ya Kiafrika ambayo italeta msisimko na mwamko mpya. Wenyeji wa Afika Mashariki na Kati wawe wa kwanza kukitambua na kukienzi Kiswahili.

Tunaendeleza ushirikiano na taasisi nyingine barani Afrika. Kwa mfano, tumeanza kushirikiana na ACALAN (African Academy of Languages) kwa manufaa ya kuiendeleza lugha ya Kiswahili kama lugha ya maeneo mapana au lingua franca. Wakati huo huo CHAUKIDU kinashirikiana na Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki. Tunashirikiana sana na taasisi nyingine kama TATAKI na BAKIZA kwa minajili ya kuboresha huduma na kuwaruhusu wanachama wetu kushirkiana na wenzao ko kote waliko duniani.

Taasisi zilizotajwa hapo juu ni za kiserikali katika ngazi za juu na tutaendelea kushirikiana nazo ili kutoa taarifa zinazoweza kusaidia katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili bila kuthiathiri lugha nyingine za Kiafrika. Na pamoja na hizi taasisi tunaamini kwamba vyama vingine vinavyoshughulikia taaluma za Kiswahili ni muhimu sana kwa malengo yetu. Kwa hivyo, tunaendelea kujenga uhusiano na ushirikiano na vyama kama vile CHAKAMA, CHAKITA, ALTA, miongoni mwa vyama vingi. Tunataka CHAUKIDU kisawiri wigo mpana zaidi.

Kila chama hakina budi kukua na kuleta mabadiliko ambayo yanaonekana sio kwa viongozi tu, bali kwa wanachama wote na wanajumuiya kwa jumla. CHAUKIDU ni chama kinachoendelea kupanua wigo wake kiutendakazi na kimtazamo. Kutokana na mazungumzo na wadau mbalimbali, ni dhahiri kwamba kazi ya bodi na wanachama wake ni kubwa mno. Kukitambulisha chama kwa jumuiya iliyo na mambo mengi na mambo mengine ya kimsingi si masihara. Hata hivyo, ikiwa tutalichukulia swala la lugha kama la kipaumbele na haki kwa binadamu ye yote yule, basi jitihada zetu zitakuwa muhimu maishani na mawazoni mwa wengi.

Kwa kumalizia basi, hebu nisisitize tena kwamba katika awamu hii ya nne lengo letu liko wazi. Tutaonesha uongozi na mwelekeo wa hekima na busara katika kuyashughulikia maswala ya taaluma za Kiswahili. Kwa sababu Kiswahili ni lugha muhimu ndani na nje ya maeneo ya Uswahilini, tutahakikisha kwamba Kiswahili kinaenziwa kote. Ughaibuni tushrikiane na balozi, taasisi, vyuo, na wanajumuiya katika kuitambulisha lugha ya Kiswahili kupitia chama. Iwe nyumbani au ughaibuni, tutakuwa na siku ya Jumuiya kama chama kutoa huduma na kwa kufanya hivyo, tukitambulishe chama zaidi. Swala la makongamano litaendelea kushughulikiwa kwa makini kwa sababu ni jukwaa la kubadilishana mawazo ya kinadharia na kiutafiti. Hata hivyo, CHAUKIDU ni chama cha wengi: wasanii, watangazaji, waandishi, wanafunzi, wanabiashara, waalimu, wataalamu, wanasera, wajasiriamali, na wadau wengine wengi ambao watahitaji kufikiwa kwa kutumia nyenzo tofauti tofauti na zinazofaa kutegemea na muktadha.

Karibuni nyote wa karibu na wa mbali tuitukuze lugha ya Kiswahili!