Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) chaukidu@gmail.com

HABARI

Taarifa Kwa Umma

Endapo haupo kwenye email list ya CHAUKIDU, naomba upokee taarifa kamili kutoka kwake Mkurugenzi mkuu wa CHAUKIDU, Prof. Leonard Muaka: WanaChaukidu, Katika ujumbe huu nitazungumzia maswala matatu muhimu.
  1. Mkutano wa DC, Mabalozi na Wanajumuiya:

Mkutano uliofanyika DC kwenye ubalozi wa Tanzania ulifana sana. Waliohudhuria walikuwa watu takriban 10. Kila mmoja alifurahi kuhusishwa kwenye shughuli za CHAUKIDU. Kwa wengi wao ilikuwa mara yao ya kwanza kusikia kuhusu chama cha CHAUKIDU. Kimsingi walipendekeza kupanua upeo wa CHAUKIDU ili chama kisjikite tu kwenye vyuo. Ingawa waliunga mkono umuhimu wa kuomba msaada kutoka balozi zetu, baadhi ya watu walitahadharisha kutegemea ufadhili kama huo. Walitusihi tufikirie njia nyingine za ufadhili au za kupata pesa kama vile kutayarisha vipindi vya madarsa ya Kiswahili mtandaoni kwa minajili ya wanachama na wanafunzi wa kibinafsi wa Kimarekani na kwingineko. Balozi zilizokuwepo ziliahidi kutusadia kadiri ya bajeti zao zinvyoweza na hata kukawa na pendekezo kutoka kwa mwanadiplomasia wa ubalozi wa DRC kwamba tufikirie namna ambavyo tuanaweza kusafiri Afrika mahali kama DRC ili kuwaelemisha walimu na wanafunzi jinsi ya kufundisha na kusoma Kiswahili kirasmi na pia kujivunia Kiswahili sanifu.

 2. Mkutano wa Wanabodi wa Tarehe 11, 2014, Athens, Georgia Kwenye mkutano wa bodi uliofanyika Athens, Georgia wanabodi wafutao walihudhuria kupitia Skype:
  • Dkt. Leonce Rushubirwa, Canada
  • Dkt. Dainess Maganda, Chuo Kikuu cha Georgia, GA
  • Prof. Lioba Moshi, Chuo Kikuu cha Georgia, GA
  • Dkt Leonard Muaka, Chuo Kikuu cha Winston Salem, NC
  • Dkt. David Kyeu, Chuo Kikuu cha California, CA
  • Bi. Beatrice Okello, Chuo Kikuu cha Indiana Bloomington, IN
  • Dkt. Rose Lugano, Chuo Kikuu cha Florida, FL
  • Bw. Patrick Mose, Chuo Kikuu cha Ohio, Athens, OH

Baada ya muhtasari wa yaliyojiri DC kutoka kwa Mkurugenzi Leonard Muaka na Mwanabodi Dainess Maganda mkutano huu ulikariri yaliyojadiliwa DC na kila mtu alipewa jukumu la kujitolea ili kufanikisha chama na miradi yake. Tulikubaliana kujigawa ili tuweze kuatekeleza mambo matatu makuu: Kushughulikia swala la kuzichanganua kata kadhaa ili kufanikisha shughuli za chama na kubuni mbinu bora za kuwavutia watu kwenye chama na kukisambaza chama na kukiunganisha chama na vyama vingine vya Kiswahili (Leonce Rushubirwa na Beatrice Okello); kuishughulikia tovuti kama njia ya kufanikisha mawasiliano (Facebook, Twitter,) ili iweze kukiwakilisha chama ipasavyo na kutumiwa kama chombo cha kuushirikisha umma kote duniani (Patrick Mose na David Kyeu); Kutafuta fedha na kuushughulikia mkutano wa DC mwakani (Rais Lioba Moshi, Mkurugenzi Leonard Muaka, na Ndugu Elias Magembe).

3. Mkutano wa mwakani na ikisiri za Kiswahili: Mipango ya mwakani DC inaendelea kushughulikiwa kikamilifu. Tunamsubiri Mwalimu Lyabaya atuambie ikiwa chuo chake cha Howard kitamruhusu kutumia ukumbi au vyumba vya hapo chuoni pake. Wakati huo huo Ndugu Elias Magembe kutoka DC amependekeza sehemu kadhaa ambazo huenda zikawa nafuu mjini DC kwa minajili ya kongamano letu. La muhimu sasa ni kuwaelekezeni ninyi wanachama namna ya kuziwasilisha iksiri zenu. Ni jambo muhimu sana kwa sababu litatusaidia katika kupangia mkutano wa mwakani.

Kila mwanachama anahimzwa kuhudhuria mkutano wetu DC ambao utafanyika tarehe 23, Aprili siku ya Alhamisi, 2015. Aidha, kila mwanachama ana uhuru wa kuhudhuria kikao kikubwa cha ALTA Dulles kuanzia Aprili 24 hadi 2, 2015. Ningependa jambo hili lieleweke na liwe wazi kabisa kwa kila mmoja wetu. Mkutano wa DC sio mbadala wa mkutano mkuu wa Dulles. Huu ni mkutano wa awali na utafuatiwa na mkutano wa Dulles kwa wale wenye mpango wa kuhudhuria NCOLCTL na ALTA 2014. Tafadhalini zingatieni mambo yafuatayo (kwa sababu yalileta utata hapo awali):

  1. Mkutano wa CHAUKIDU DC utakuwa na utawahusisha wanazuoni, mabalozi, wanajumuiya, na wanahabari. Tungependa kuwa na meza tofauti zitakazowaruhusu hadhira kushiriki ipasavyo. Ili kuwasilisha itabidi iksiri zenu zifikie kamati ya maandalizi ya CHAUKIDU 2015 kabla ya Novemba 03, 2014. Ikisiri husika zitumwe kwa Mkurugenzi kupitia anwani ifuatayo: muakale@wssu.edu
  2. Tunapendekeza (kwa mkutano wa DC) $50:00 za usajili na ada ya uanachama kutegemea viwango vya uanachama wa CHAUKIDU. Malipo ya usajili yafanywe kabla ya Februari 16, 2015. Chaukidu itaendelea kulipa ada ya chama kwa ALTA kwa ajili ya mkutano wa Dulles Airport kwa wale ambao watapenda kuwasilisha huko. Tafadhali zingatia kwamba ada za mkutano na uanachama wa ALTA huko Dulles Airport zitahusu chama cha ALTA tu.
  3. Kwa sababu ninajua kuna wengine wetu ambao watashiriki na pia kuwasilisha makala yao katika kongamano kuu kule Dulles Airport, nawaombeni mzitume ikisiri zenu kwa kufuata kanuni/taratibu na maelekezo ya Secretariat ya ALTA ambayo yanaweza kupatikana kwenye mtandao wa ALTA < ALTA link > au jumbe kadhaa ambazo wamekuwa wakituma.

Asanteni kwa michango yenu ambayo itatusaidia kufanikisha mipango na malengo yetu. Kama kawaida kama kuna ye yote ana swali au maoni, unakaribishwa kuchangia.

Leonard Muaka Mkurugenzi Kwa niaba ya Bodi ya CHAUKIDU