Rais

Dr. Mahiri Mwita Rais

Mahiri Mwita, PhD
Rais wa Chaukidu
Chuo Kikuu cha Princeton

Nina furaha na hamasa kubwa kujiunga na bodi ya awamu ya tatu ya CHAUKIDU. Kwanza niwapongeze na kuwashukuru marais, wakurugenzi na wanabodi wa awamu ya kwanza na ya pili walionitangulia, kwa kukizindua chama cha CHAUKIDU, na pia kwa kukilea na kukipa miguu na mikono ambayo hivi leo inatupa nguvu ya kutambaa na kuanza kusikika kote ulimwenguni, kuanzia hapa Marekani kilipoasisiwa chama, hadi nyumbani Afrika Mashariki na kwingineko kote duniani.

Kama walivyonena watangulizi wangu wa bodi inayoondoka, “… Lengo kuu la chama (cha CHAUKIDU) ni kuwaunganisha wapenzi wa Kiswahili po pote walipo duniani ili kwa pamoja tuweze kukidumisha Kiswahili na kuhakikisha kinashika nafasi maalum katika orodha ya lugha za dunia.”

Kwa mintarafu hii, kwa niaba ya bodi ya awamu ya tatu ya CHAUKIDU, ninataka kupiga mbiu kwa wadau wote wa Kiswahili duniani wachangamkie juhudi hizi ndogo za CHAUKIDU za kutoa nafasi kwetu sisi wote tunaokunwa na kukereketwa na lugha, fasihi, utamaduni au hata na mazingira ya eneo linalijivunia Uswahili, kujitokeza na kujiunga nasi katika kutafuta, kuvumbua na kudumisha mikatakati ya kuendeleza Kiswahili na Uswahili dunianai.

CHAUKIDU imeasisiwa ughaibuni hasa Marekani katika mwongo wa kwanza wa miaka ya 2000. Mojawapo ya sababu za usuli huu ni kwamba hivi sasa serikali na vyuo vingi katika nchi za Marekani Kusini, hasa Umarekani na Kanada, pamoja na nchi za Uropa, Uchina na Ujapani zimetambua umuhimu wa kujifunza lugha za kigeni kama nyenzo ya kupenya na kuufahamu utamaduni na utu wa jamii nyinginezo wanazotangamana nazo duniani kisiasia, kiuchumi na kitamaduni. Kwa mfano, nchini Marekani, baada ya pigo la kigaidi la 9/11, serikali na taasisi za kiserikali, kiusalama na kielimu zilizinduka na kugundua kwamba pamoja na ubabe wake duniani, jamii na taasisi za Kiamarekani hazikujua lolote kuhusu utamaduni wa jamii nyingi walizojihusisha au kutangamana nazo duniani. Waligundua kwamba walikuwa mbumbumbu, hata hawakuwa na wataalamu wa kutosha walioweza kuwashauri kuhusu tamaduni za nchi nyingi walizotangamana na hata kupigana nazo kama vile Iran, Iraq, na Afghanistan katika Uarabuni, au hata India, Ujapani na Uchina katika Mashariki ya Mbali.

Utambuzi huu umepelekea serikali, vyombo vya usalama na taasisi za elimu kuupa mradi wa ufundishaji wa lugha za kigeni kipaumbele katika programu zao. Hili limewezesha kuwepo kwa program nyingi za ufundishaji wa lugha za kigeni Ughaibuni. Katika Marekani na Uropa, Kiswahili kimekuwa mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo na taasisi nyinginezo za elimu kuanzia elimu ya sekondari hadi vyuoni. Mwamko huu mpya umeongeza maradufu umaarufu wa Kiswahili katika mradi huu wa Lugha za Kigeni Ughaibuni, na kuifanya kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika inayofundishwa katika vyuo na taasisi nyingi zaidi katika Marekani Kaskazini, Uropa, maeneo mengi ya Afrika nje ya Afrika Mashariki, na Mashariki ya Mbali. Maendeleo haya hayachangii tu umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa taasisi na wenyeji wa nchi za ughaibuni, bali pia yanazalisha jamii mpya ya “Waswahili” ambao wanadai nafasi katika meza ya “washika dau” wa Kiswahili.

Pamoja na hili, kuna Waswahili wengi sana wanaokaa ughaibuni hivi leo – kwa maana ya wenyeji wa Afrika Mashariki ambao si tu wanatoka nchi-asili za Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya na Uganda), bali pia majirani kutoka Kongo, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini, Sudani Kusini na Somalia ambako Kiswahili kimeibukia kuwa lingua franka kutokana na sababu za vita na mustakabali mbalimbali wa kisiasa, kiuchumi na kijamii unaounganisha watu wa maeneo haya na lugha ya Kiswahili. Kwa mfano huku ughaibuni, mtu yeyote wa asili ya Kenya au Tanzania (kunakozungumzwa Kiswahili kama lugha ya kila siku) anapokutana na mwenzake wa asili ya Somalia, Kongo au Sudan Kusini, kinachowaunganisha ni lugha ya Kiswahili na tajriba yao katika nchi-asili za Afrika Mashariki. Umma huu ni sehemu muhimu ya jamii ya “Waswahili” wa ughaibuni ambao lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Afrika Mashariki ni kipengele cha msingi cha utambulisho wao katika mustakabali wao mpana wa kijamii katika Marekani au kwingineko ughaibuni.

Mumo humo katika jamii hii ya “Waswahili” wa ughaibuni, kuna wasomi na wataalamu ambao wamekuja ughaibuni kwa sababu za kielimu – kusoma taaluma, iwe ya Kiswahili au elimu nyingineyo. Kundi hili linaweza kugawanyika kuwili: wale waliotoka Afrika Mashariki kuja ughaibuni kusoma taaluma nyinginezo kama vile sayansi, sayansi-jamii, na sanaa-jamii. Katika kundi hili kuna wengi, hasa kuanzia miaka ya sitini hadi tisini ambao walipokuja ughaibuni waliajiriwa kama walimu wasaidizi wa kufundisha Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika, kama mojawapo ya nyenzo ya kugharamia masomo yao katika vyuo vya ughaibuni. Ingawa wengi wa kundi hili huwa hawajitambulishi na “taaluma” ya Kiswahili, hao ndio walikuwa “walimu” wa Kwanza wa Kiswahili kama somo na taaluma ya kufundishwa katika vyuo vya ughaibuni.

Kwa upande wa pili wa kundi hili la "Waswahili-wasomi" wa ughaibuni, kuna wanafunzi, walimu, na watalaamu wa lugha, isimu, fasihi na athropolojia ya Kiswahili walioko katika shule, vyuo na taasisi za elimu kote katika dayaspora. Kundi hili limepanuka kwa kasi sana katika miaka ya kuanzia tisini kwa sababu kadha. Licha ya sababu ya uhitaji wa wataalamu wa Kiswahili kwa ajili ya vyuo vya ughaibuni vinavyokipa kipaumbele Kiswahili, kuna sababu za kinyumbani pia. Mojawapo ni kupanuka kwa elimu ya juu Afrika Mashariki na athari yake ya kuwatuma wataalamu wengi nje ya Afrika mashariki kusomea digrii za juu. Aidha, taaluma ya Kiswahili katika vyuo na taasisi za elimu katika Afrika Mashariki imepanuka sana kiasi kwamba hiivi leo takribani kila chuo Afrika Mashariki kinafundisha Kiswahili siyo tu kama somo na lugha ya taifa, bali pia kama taaluma inayotafitiwa hadi shahada za uzamili na uzamifu. Hali hii imechangia katika kuzalisha kundi kubwa la wasomi wa Kiswahili wanaosoma au kufanya kazi katika vyuo na taasisi za elimu ughaibuni.

Hili ndilo kundi ambalo hii leo linatafuta ungo wa kuunganisha usomi wa taaluma ya Kiswahili ughaibuni na ule wa nyumbani Afrika Mashariki na kwingineko ulimwenguni. CHAUKIDU ni tokeo muhimu la juhudi za kundi hili.

Kwa hivyo, hii leo tunapozungumzia wadau na wakereketwa wa Kiswahili, tunajaribu kuzifikia, kuzishirikisha na kuziunganisha jamii hizi zote za “Waswahili” katika mradi wa kukifurahia Kiswahili sio tu kama nyenzo muhimu ya utambulisho wetu duniani, lakini pia kama chombo cha mawasiliano, chombo cha ajira, chombo cha kitaaluma na kiakademia katika soko kubwa la kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kitaaluma linalozalishwa na Kiswahili nyumbani na ughaibuni. Na kwa sabau Kiswahili kinasema kwamba “mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani”, sisi katika CHAUKIDU tunajituma na kujipa majukumu ya kuwezesha, kupanua, kuboresha na kukarihisha ushikiano na utangamano wa Waswahili wote popote walipo, iwe nyumbani Afrika Mashariki, kwingineko Afrika au ughaibuni na dayaspora zetu zote ulimwenguni.

Karibuni sana, na kwa niaba ya bodi ya CHAUKIDU, nakuomba wewe Mswahili wa aina yoyote na popote ulipo tushikane mikono na kuendeleza Kiswahili na utamaduni wetu.

KARIBUNI WOTE