CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Wasiliana Nasi

Mitandao ya Jamii

Jarida la CHAUKIDU

Jarida la CHAUKIDU ni jarida la kitaaluma linalochapishwa na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani na kusambazwa katika nakala ngumu na nakala tepe. Jarida hili ni la kitaaluma na linachapishwa mara moja kwa mwaka. Jarida hili linachapisha makala juu ya taaluma za Kiswahili ambazo hazijachapishwa kwingine wala hazijawasilishwa kuchapishwa katika jarida jingine au machapisho mengine.  Makala za jarida hili zitatahakikiwa  kwa kufichisha ambapo watakaotahakiki hawatamjua mwandishi wa makala. Kufanya hivi kunapunguza upendeleo au hisia zinazowahusu watu binafsi. Jarida hili linapatikana bure katika tovuti hiyo. Malengo Lengo kuu ni kuwahusisha na kuwashirikisha wanazuoni wa Kiswahili na wapenzi wa lugha hiyo duniani kote katika kubadilishana maarifa na maoni. Ukuaji na usambaaji wa Kiswahili, na hadhi mpya inayopata Kiswahili kama lugha rasmi inakuza haja ya wataalamu wa Kiswahili kujadili na kupashana maarifa kwa mapana zaidi. Kwa kuwaunganisha wataalamu wabobezi na wale wanaoibukia jarida linakusudia kuwajengea wanataaluma wanaoibuika utamaduni wa kuandika na kubadilishana mawazo kitaalamu katika viwango vya kimataifa. Mchango mmoja wa jarida hili ni kuimarisha ushiriki wa wataalamu wa Kiswahili katika midahalo, malumbano na ukuzaji wa maarifa ya Kiswahili kimataifa. Lengo jingine la Jarida kuweka daraja baina ya kazi ambazo ni za kiufafanuzi zaidi na zile ambazo ni za kinadharia. Jarida hili litapokea michango ya kitaaluma kutoka mikabala mbalimbali ya kinadharia na kimethodolojia. Upeo Jarida hili litachapisha makala za kitaalamu za fasihi, isimu, na utamaduni wa Kiswahili. Taaluma mbalimbali katika tanzu za kimapokeo na pia tanzu mpya zinazoibuka hasa kutokana na maendeleo ya teknolojia.
  1. Ufundishaji wa lugha
  2. Isimu: km fonetiki, fonolojia, mofolojia, semantiki, isimu linganishi, isimu jamii, nk
  3. Fasihi: fasihi simulizi, fasihi andishi,
  4. Ulinganifu wa Kiswahili na lugha nyingine za Afrika.
  5. Utamaduni wa Waswahili na wazungumzaji wa Kiswahili
  6. Sera na matumizi ya lugha
  7. Maendeleo ya Kiteknolojia
Aina za makala Tunatoa mwito kwa makala mbalimbali na tunapokea makala wakati wowote ule. Makala zitakazopewa kipaumbele ni:
  1. Makala za kiutafiti zenye kuonesha matokeo ya uchunguzi, midahalo, nk
  2. Tahakiki za kazi za fasihi, sanaa na kazi nyingine
  3. Makala zanazoelezea na kufafanua mbinu za ufundishaji wa lugha
  4. Makala chokonozi ndefu au fupi
  5. Tahakiki fupi za vitabu visivyo vya fasihi
  6. Makala au orodha za istilahi mpya
  7. Makala kuhusu maendeleo ya teknolojia na lugha ya Kiswahili