CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Wasiliana Nasi

Mitandao ya Jamii

Kongamano la CHAUKIDU 2016

Kongamano la nne la mwaka 2016 la Chaukidu limepangwa kufanyika jijini Atlanta, GA. Kongamano hili litawahusisha na kuwaleta pamoja wakufunzi wa Kiswahili, watafiti, wanafunzi, wanahabari, wasanii, wanaharakati, wanafasihi, wachapishaji, wahudumu wa utalii, taasisi mbalimbali, wakereketwa na wadau wa Kiswahili toka sehemu mbalimbali duniani. Kongamano pia litawaleta wazungumzaji wazawa wa Kiswahili ambao wanaishi katika maeneo yanayolizunguka jiji la Atlanta pamoja na maeneo mengine ya Marekani.

Chaukidu ingependa kutumia mkutano wa mwaka huu kukizindua chama hiki rasmi, na kutambulisha umuhimu wake kitaifa na kimataifa. Mgeni rasmi, ambaye atafanikisha zoezi hili la uzinduzi atakuwa Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Mwinyi, hata baada ya urais, amekuwa miongoni mwa viongozi wakubwa wachache waliojiweka mstari wa mbele kukipigania Kiswahili pamoja na utamaduni wake, na ametupatia heshima kubwa kwa kukubali kuhudhuria kwenye kongamano letu la mwaka huu. Mkutano pia utawahudhurisha mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali walioko nchini Marekani wakiziwakilisha nchi za Afrika Mashariki na Kati pamoja na jumuiya mbalimbali za Kiafrika.

Rais, Mkurugenzi, na wanabodi wote wa Chaukidu wanayo furaha kuwakaribisha wadau wote wa Kiswahili na utamaduni wake katika kongamano hili.