Mada za Kampala 2019
Hoja ya kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha za mawasiliano mapana (lingua francas)
katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati, ni suala ambalo halihitaji mjadala. Hata
hivyo, kwamba lingua francas huambatana na faida na hasara au huwa na athari chanya
na hasi katika jamii husika, ni madai ambayo yameibua mjadala mkali ndani na nje ya
wigo wa kiakademia duniani kote. Mjadala huu uko hai, unaendelea na unataka majibu.
Mintaarafu mjadala huu, Kongamano la tano la kimataifa la CHAUKIDU linalenga kutoa fursa ya kuvinjari na kutafakari kwa kina kuhusu uhusiano uliopo kati ya ukuaji wa Kiswahili na ustawi au uviaji (udumazaji) wa lugha nyingine za Kiafrika katika ukanda wa Afrika ya
mashariki. Kwa kufanya hivi, Kongamano hili litakuwa limetoa mchango mkubwa katika
mjadala mpana ambao hatimaye matokeo yake yanaweza kuwa na manufaa ya kitaaluma, kisera, kijamii, na hata kimtazamo katika maisha ya kila siku ya wanajamii wa Afrika ya Mashariki.na kwingineko duniani.
Sambamba na lengo hilo hapo juu, Kongamano la tano la kimataifa la CHAUKIDU
litakalofanyika jijini Kampala, nchini Uganda linalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa Kiswahili duniani kote ili kujadili uendelezaji na unawirishaji wa Kiswahili na lugha nyingine za Afrika Mashariki. Ni matarajio yetu kuwa wadau wengi wa Kiswahili watachangamkia fursa ya kujadili na kuchangia masuala haya kupitia mawasilisho, na mazungumzo na pia ni matumaini yetu kuwa mijadala hii itachochea uendelezaji wa lugha yetu adhimu ya Kiswahili pamoja na lugha zetu nyingi zinazozungumzwa katika eneo la Afrika ya Mashariki na Kati.
Kwa kuhitimisha, Kongamano hilo litawapa fursa wapenzi na wakereketwa wa Kiswahili,
walimu, wanafunzi, watafiti, waandishi, wanahabari, wanasiasa, wasanii, wakuzaji wa mitaala, maafisa wa lugha, wachapishaji, wanasayansi, wafanyabiashara, n.k., kubadilishana na kuelimishana kuhusu maarifa, weledi, tajiriba, taaluma n.k. zinazohusiana na lugha ya Kiswahili.
Kongamano litakuwa na mada ndogondogo kama ifuatavyo:
- Kiswahili na siasa/utawala/uongozi (usalama, ulinzi, uhamiaji, diplomasia, nk)
- Kiswahili na utamaduni (jadi, imani za kidini, michezo, ujenzi, mavazi, vyakula, mapishi, nk)
- Kiswahili na uchumi (biashara, viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, madini, miundombinu)
- Kiswahili na elimu (ngazi za elimu, lugha ya kufundishia/kujifunzia, taaluma, tafiti, uchapishaji)
- Kiswahili na Sanaa (muziki, maigizo/filamu, vibonzo, nk)
- Kiswahili na fasihi (nadharia, simulizi, andishi, riwaya, ushairi, tamthiliya, nk)
- Kiswahili na isimu (maumbo, miundo, nadharia, nk)
- Kiswahili na lugha za Kiafrika (kujengana, kukamilishana, nk)
- Kiswahili na upashaji habari (magazeti, vijarida, redio, runinga, mitandao ya kijamii, blogu, nk)
- Kiswahili kwa wageni (Afrika, Ulaya, Asia, Amerika, nk
- Kiswahili na lahaja zake (Kiswahili cha mitaani, kiSheng, kiSwanglish, nk.)
- Kiswahili na teknolojia na utandawazi
- Kiswahili na uhamasishaji, uenezi (maarifa, itikadi, teknolojia, nk)
- Kiswahili na vyama vya ushirika na maendeleo yake
- Utafiti wa Kiswahili na taaluma zake