MADA KUU: HALI YA KISWAHILI ULIMWENGUNI SASA NA BAADAYE
Kiswahili ni miongoni mwa lugha za Kiafrika na za Kimataifa inayozungumzwa na watu takriban milioni 150 ndani na nje ya bara la Afrika. Pia, ni lugha inayotumika katika kutekeleza majukumu anuwai yakiwemo elimu, siasa, biashara n.k. Katika mkabala huo, Kiswahili kinaibuka kama Lingua Franka Afrika Mashariki na mataifa kadha barani Afrika. Mbali na kuwa lugha muhimu Afrika, Kiswahili kinatumika pia kote ulimwenguni kwa namna moja au nyingine, kwa mfano katika ufundishaji, uanahabari, utafiti, uanaharakati, n.k. Kwa mantiki hiyo, na kutokana na matukio ya sasa duniani, Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kinapanga kuandaa kongamano litakalozungumzia hali ya ufundishaji wa Kiswahili ulimwenguni kwa sasa, hasa kipindi hiki cha Korona na athari zake katika siku za usoni. Kongamano hili ambalo litafanyika mtandaoni, litawaleta pamoja wataalamu wa Kiswahili kutoka Afrika pamoja na mataifa mengine ulimwenguni kubadilishana mawazo.
Mada Ndogo:
- Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili katika Kipindi cha Janga la Korona.
- Kiswahili na Maendeleo Endelevu katika Jamii.
- Kiswahili na Teknolojia
- Kiswahili na Mazingira ya Ufundishaji/Ujifunzaji
- Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Pili/Kigeni
- Ubunifu na Ugunduzi katika Ufundishaji wa Kiswahili wakati wa Korona
- Kiswahili, Elimu na Afya.
- Uundaji, Usambazaji na Usawazishaji wa Istilahi za Kiswahili.
- Pedagojia katika Taaluma za Lugha, Isimu na Fasihi
- Utafiti, Uandishi na Uchapishaji wa Vitabu vya Kiswahili
Ikisiri zote zitumwe kwa kujaza fomu maalumu ya ikisiri inayopatikana kwa kufungua kiungo hiki au kwa kubofya 'Ikisiri' katika vitufe vilivyoko upande wa kushoto. Kwa swali lolote kuhusu kongamano hili la Mei la Mtandaoni, wasiliana na Kamati-Andalizi kupitia barua-pepe hii: kongandao2021@gmail.com.