CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Wasiliana Nasi

Mitandao ya Jamii

Mkurugenzi 2016

Leonard Muaka, PhD

Mkurugenzi Chaukidu
Chuo Kikuu cha Howard

Kwa Jumuiya ya Waswahili kote Duniani

Fursa hii ni kwenu ninyi nyote wapenzi wa Kiswahili Afrika, Uropa, Uchina, Amerika, Uarabuni na pembe zote za dunia ambako wanadamu huwasiliana. Dunia ya sasa inaunganishwa na lugha. Inaweza kuwa ni lugha ya kimaandishi au ya kimaongezi. Kwa vyo vyote vile Kiswahili ni moja ya lugha maarufu na muhimu katika dunia ya sasa. Mchango wetu kama wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili, wakereketwa wa lugha ya Kiswahili, na watalaamu wa lugha ya Kiswahili, ni kuitetea na kuisambaza kupitia vyombo vya kisasa. Kiswahili kitanawiri miongoni mwa vizazi vya sasa na vijavyo kupitia jitihada ya kila mmoja wetu.

Ni uchungu mkubwa kwa mzazi wakati anapoulizwa na binti yake, “baba, kwa nini hukunifundisha Kiswahili au lugha yako?” Kama mzazi, utatoa sababu kadhaa lakini ukweli ni kwamba pamoja na haki nyingi ambazo dunia ya sasa inatutarajia tuwahakikishie watoto na wanajamii, haki moja muhimu ni lugha. Tuwapeni vijana wetu lugha. Tusisahau kwamba wingi lugha au kufahamu lugha kadha ni dafina lakini pia ni kitu kinachohitajika sana katika dunia hii ya sasa na hata tafiti zimeonyesha kwamba wingi lugha hupanua fikra za mtu.

Kwako wewe kama msomaji wa makala hii, CHAUKIDU ni chama kinachokupa fursa hii. Jumuika na wapenzi wa lugha ya Kiswahili  kutoka kote duniani ili tuienzi lugha yetu na kuipa nafasi yake stahiki katika ulimwengu wa sasa. Kiisimu hakuna lugha duni, na basi tusiwe ni sisi wenyewe tutakaokidunisha Kiswahili. Tusisahau alichokisema Shaaban Robert, “titi la mama li tamu, lijapokuwa la mbwa.”

Kiswahili chahitaji mchango wa wadau wote, wakiwa mtu mmoja mmoja au makundi, ama asasi. Kwa hiyo twatoa wito kwako kuchangia kusambaa kwa Kiswahili kwa hali na mali kwa sababu una uwezo, nia, na  fursa ya kufanya hivyo. Ukiwa na swali au hoja yoyote ile, changia kwenye blogu ya CHAUKIDU au tuma barua pepe kwa mwakilishi wako, au mkurugenzi, au hata rais wa chama. Tuko hapa kukutumikia lakini bora tushirikiane kutekeleza lengo letu moja – kukikuza na kukisambaza Kiswahili kote duniani.

Leonard Muaka, PhD

Mkurugenzi