Kwa miaka mingi, uchapishaji wa vitabu vya vya taaluma mbalimbali umekuwa ukifanyika kwa lugha ya Kiingereza, na hii imesababisha matini na vitabu viwalengavyo wasemaji wa Kiswahili kutokuifikia hadhira iliyokusudiwa kwa sababu vimeandikwa katika wasiyoimudu vyema. Vilevile, kwa miaka mingi, wapingaji wa matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, wamedai Kiswahili hakifai kuwa lugha ya kufundishia kwa sababu vitabu, matini, na majarida ya Kiswahili yanayoweza kutumiwa kufundishia hayatoshelezi mahitaji. CHAUKIDU Press au Matbaa ya CHAUKIDU imeundwa ili kuziba pengo hilo. Matbaa ya CHAUKIDU itaendeleza malengo ya CHAUKIDU kwa kuchapisha vitabu mbalimbali na majarida ya kitaaluma kwa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kukata kiu ya wasomaji na wasemaji wa Kiswahili walionea kote duniani. Matbaa itachapisha vitabu vya taaluma za Kiswahili, kazi bunilizi (kama riwaya, tamthiliya, na ushairi), na vitabu vya taaluma nyingine kama Biolojia, Fizikia, Anthropolojia, n.k. Kwa ujumla. machapisho haya yataandikwa na waandishi na wasomi wa kitaifa na kimataifa wanaowakilisha mitazamo anuwai ya kielimu na kitaaluma. Katika kutimiza dhamira yake, waandishi watatoka katika makundi ya kitaaluma yakiwemo yafuatayo:
- Fasihi ya Kiswahili
- Isimu ya Kiswahili
- Isimu ya lugha nyingine
- Utamaduni
- Kamusi za Kiswahili <> Lugha nyingine
- Sera
- Elimu
- Teknolojia na Kompyuta
- Siasa
- Sheria na Uanaharakati
- Maendeleo ya Mitaala
- Maendeleo ya Kitaaluma
Tunakaribisha miswada ya vitabu vipya. Kuwa miongoni mwa wataalamu wa kwanza watakaochapisha na CHAUKIDU Press. Ukiwa na makala ya jarida, tuma makala yako pia ili ifanyiwe tathmini na kutoka katika matoleo yetu yajayo ya Jarida la Chaukidu.