CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Kuhusu Chaukidu

Kuhusu CHAUKIDU

Chama hiki, CHAUKIDU, kimeanzishwa baada ya miaka mingi ya kuomba, maandalizi, na mijadala mingi miongoni mwa wapenzi wa Kiswahili kutoka maeneo mbalimbali duniani, ambao wote walikuwa na hamu ya kuona uanzishwaji wa jumuiya ya watu watakaokuwa tayari kujitoa mhanga kwa kushirikiana na taasisi na jumuiya nyingine kukiendeleza na kukitangaza Kiswahili katika nyanja zote ili kukiletea heshima ndani na nje ya Afrika. CHAUKIDU kilizinduliwa na katiba yake kupitishwa katika mkutano uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Wiskonsin mnamo tarehe 26 Aprili, 2012.

Kwa mujibu wa katiba yake, Makao Makuu ya CHAUKIDU kwa sasa yako katika Chuo Kikuu cha Georgia, nchini Marekani, ambako Rais wa sasa huishi na kufanya kazi, hadi hapo atakapostaafu au awamu yake itakapokwisha. Chama kilianzishwa kikiwa na malengo ya kuhimiza na kuharakisha maendeleo ya iswahili duniani kote.

Malengo ya CHAUKIDU

Kutangaza lugha ya Kiswahili maeneo yote duniani na kuongeza mahusiano kati ya maeneo hayo na Afrika Mashariki, lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili. Vilevile, chama kina malengo ya kuwaunganisha wadau wa Kiswahili waliotawanyika kwenye pembe nne za dunia.

Madhumuni ya CHAUKIDU

Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.

  1. Kuwaunganisha wanachama wote kwa malengo ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika maswala mbalimbali yahusianayo na Kiswahili (mfano. mbinu za ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi n.k.) kwa kuratibu makongamano ya kila mwaka, washa, makongamano maalumu, na makongamano ya mitandaoni.
  2. Kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kujivunia kuwa Mswahili, kuendeleza na kuitangaza fahari ya Kiswahili.
  3. Kuzishauri na kuzihimiza serikali za nchi ambazo Kiswahili huzungumzwa kuitambua thamani ya Kiswahili ili kufanya yote yawezekanayo katika kuunda sera madhubuti ambazo zitahakikisha maendeleo ya Kiswahili kijamii, kisiasa na kiuchumi, na kuuendeleza utamaduni wa watu wake.