CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Mada Kilifi 2021

Mada za Kilifi 2021

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mjadala mkali miongoni mwa wanazuoni, wataalamu, watumiaji, na wanafunzi wa Kiswahili kuhusu ‘Kiswahili Sanifu’ na aina nyingine za uzungumzaji au/na uandishi wa Kiswahili hususani kwa kuzingatia mipaka ya utaifa (kama vile Kenya, Tanzania visiwani na Tanzania bara, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kwingineko) na hata mipaka ya miktadha ya kijamii (kama vile mitaani, shuleni, tahariri, michezo, na kadhalika).

Tunapoingia muongo wa mwisho kabla ya maadhimisho ya miaka mia moja tangu kuanzishwa rasmi kwa shughuli za usanifishaji wa Kiswahili, ni wakati muafaka na jambo wa Kiswahili kuhimizana kuanza ama kuendeleza tafiti za kina na makini kuangazia suala hili la ‘Kiswahili sanifu’ na mkabala wa ‘Viswahili vingine’. Hii itasaidia, hadi tufikapo wakati wa maadhimisho ya karne moja ya usanifishaji (mwaka 2030), kuwepo na data na machapisho kuntu ambayo yataweza kutoa dira ya miaka mia moja mingine ijayo. Kongamano la CHAUKIDU la mwaka wa 2021 litakalofanyika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi Kenya limedhamiria kuwa jukwaa la kupuliza kipenga kuhusu mchakato huu.

Sambamba na lengo hilo hapo juu, Kongamano la sita la kimataifa la CHAUKIDU litakalofanyika mjini Kilifi, nchini Kenya linalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa Kiswahili duniani kote ili kujadili uendelezaji na unawirishaji wa Kiswahili na lugha nyingine za Afrika Mashariki. Ni matarajio yetu kuwa wadau wengi wa Kiswahili watachangamkia fursa ya kujadili na kuchangia masuala haya kupitia mawasilisho, na mazungumzo, na pia ni matumaini yetu kuwa mijadala hii itachochea uendelezaji wa lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Kongamano hili litawapa fursa wapenzi na wakereketwa wa Kiswahili, walimu, wanafunzi, watafiti, waandishi, wanahabari, wanasiasa, wasanii, wakuzaji wa mitaala, maafisa wa lugha, wachapishaji, wanasayansi, wafanyabiashara, n.k., kubadilishana na kuelimishana kuhusu maarifa, weledi, tajiriba, taaluma n.k. zinazohusiana na lugha ya Kiswahili.

Kamati-andalizi ya kongamano la CHAUKIDU la mwaka huu inakaribisha ikisiri za makala/tafiti zinazoangazia mada hii. Tafiti/makala zinaweza kuangazia usanifishaji wa Kiswahili, mchango, na changamoto zake katika nyanja anuai kama vile:

  1. Fasihi ya Kiswahili (andishi na simulizi)
  2. Isimu (Sintaksia, Mofolojia, Fonolojia, Semantiki,   Pragimatiki, Leksikografia, Elimulahaja n.k)
  3. Isimujamii
  4. Tafsiri
  5. Ukalimani
  6. Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA)
  7. Uandishi wa habari na utangazaji
  8. Uchapishaji katika Kiswahili
  9. Ufundishaji wa Kiswahili shuleni na vyuoni
  10. Ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni
  11. Kiswahili na Siasa (ushirikiano, utawala bora, demokrasia na maendeleo)
  12. Filamu, komedi futuhi), na vibonzo
  13. Muziki (bongofleva, taarabu, injili, nk)
  14. Kiswahili na lugha ya/za kufundishia
  15. Kiswahili na Lugha za jamii ndogondogo
  16. Kiswahili na tamaduni-pendwa
  17. Lugha na Utamaduni
  18. Lugha nyinginezo na usanifishaji wa Kiswahili
  19. Uundaji wa istilahi na msamiati wa Kiswahili