CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Blog Details

CHAUKIDU Arusha 2023: Mwito wa Ikisiri

Mnasaba wa Kiswahili na Nyuga Nyingine

Dira ya Mustakabali

Kiswahili kinazidi kupaa na kupata heshima kote duniani kwa  sasa. Mwaka 2021 Kiswahili kiliingia katika rekodi nyingine mpya ya kupewa siku maalumu ya kuadhimishwa ambayo ni tarehe saba Julai kila mwaka. Suala hili lilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) tarehe 23/11/2021 huko Paris nchini Ufaransa katika Mkutano wa 41 wa nchi wanachama wa shirika hilo. Kadiri lugha yoyote inavyotamalaki na kupata mashiko zaidi duniani, ni kawaida lugha hiyo kunasibiana na nyuga nyingine za kimaisha. Kutokana na kutambua vema suala hilo, CHAUKIDU kimeamua kualika wadau wa lugha ya Kiswahili kuandaa makala kuhusu dira na mustakabali wa Mnasaba wa Kiswahili na Nyuga Nyingine  kisha kuwa na mjadala wa kina utakaoongeza fursa za Kiswahili pamoja na kuchangia kuipa nafasi zaidi lugha hiyo adhimu ya Kiswahili. Majadala huo unategemewa kufanyika katika Kongamano la Nane la Kimataifa la CHAUKIDU, litakalofanyika huko mjini Arusha Tanzania, katika chuo cha MS TCDC.

Kwa hiyo, tunawaalika wanazuoni na wadau wa Kiswahili kwa ujumla kutuma ikisiri za makala kuhusu mada kuu ya Kongamano huku wakimakinikia mada ndogondogo zifuatazo:

  • Kiswahili na siasa
  • Kiswahili na uchumi
  • Kiswahili na maarifa asilia
  • Kiswahili na lugha mama
  • Kiswahili na elimu
  • Kiswahili na vyombo vya habari
  • Kiswahili na tafsiri/ukalimani
  • Kiswahili na Utalii
  • Kiswahili na teknolojia
  • Kiswahili na biashara
  • Kiswahili na lugha nyingine
  • Kiswahili na utamaduni
  • Kiswahili na michezo
  • Kiswahili na uga mwingine wowote atakaopendezewa na mwandishi wa makala

Maelekezo ya Ikisiri

Kutuma au kufanyia tathmini ikisiri, utapaswa uwe na akaunti katika mfumo wetu wa ikisiri wa Kongamano la Arusha 2023. Ikiwa bado huna akaunti katika mfumo/tovuti yetu, tafadhali tengeneza akaunti kwa kutumia anuani-pepe yako na nywila utakayoichagua. Katika uandishi wa ikisiri, tafadhali zingatia yafuatayo:

  1. Anuani/Kichwa cha Ikisiri Kichwa cha ikisiri kiwe kinaeleweka vizuri. Kisipungue maneno matano na kisizidi maneno 20. Kisiwe na isitilahi za kiujumla sana (mf. Kiswahili na TEHAMA). Kiwe kinaendana na maudhui ya wasilisho yaliyobainishwa katika ikisiri.
  2. Maudhui ya Ikisiri Maudhui ya Ikisiri ndiyo hasa kiini cha tathmini. Maudhui yawe na maneno yasiyozidi 150 na yawe yanagusia mada kuu na moja ya mada ndogondogo za kongamano hili. Sehemu kubwa ya maamuzi ya tathmini itajiegemeza katika kipengele hiki. Utapewa sehemu ya kuchagua mada ndogo inayoendana na wasilisho/ikisiri yako.
  3. Lugha ya Uandishi Mwandishi atumie lugha fasaha na inayokubalika katika muktadha wa kitaaluma. Ikisiri isiwe na makosa ya kitahajia na iwe na mtiririko mzuri wa mawazo.
  4. Usiandike Majina Yako Tathmini zitafanyika katika mfumo wa ‘double blind’. Mtathmini hapaswi kujua jina la mwandishi wa ikisiri anayoitathmini. Hivyo, katika ikisiri yako, usiandike majina yako popote. Ukishajisajili kwenye mfumo, tutajua ikisiri hiyo imetumwa nawe, ila usiweke majina kwenye ikisiri yenyewe, au kwenye kichwa/anuani ya ikisiri. Kama utaweka kiambatisho chochote, usiandike majina yako humo pia.
Releted Tags
    Share:

    Leave a comment