Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa CHAUKIDU
Wapendwa Wanachama wa Chaukidu, Kama mjuavyo, kila baada ya miaka miwili, chama chetu hufanya uchaguzi mkuu kuwachagua viongozi na wajumbe wa Bodi ya Utendaji kama ilivyoainishwa katika katiba yetu. Mwaka huu, 2021, ni mwaka wa uchaguzi na wanachama hai watapata fursa ya kuchagua na kuchaguliwa viongozi watakaounda bodi mpya ya CHAUKIDU kwa miaka miwili ijayo. Mwenyekiti wa Tume ya Katiba na Uchaguzi (TKU), ndugu Dkt. Elias Magembe amenipatia tangazo nililoliambatisha hapo chini. Tangazo hilo linatoa taarifa ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi ambao utasimamiwa na kamati/tume aiongozayo Dkt. Magembe. Mwenyekiti Ndugu Magembe ameniomba nisisitize kwamba ni WANACHAMA HAI pekee watakaopewa ruhusa ya kupiga na kupigiwa kura. Katika barua-pepe yake kwangu amesema, “tunaomba ofisi yako itutumie orodha ya wanachama wote wa CHAUKIDU, ikionyesha walio hai na hata wasio hai. Hii itatusaidia kusasisha daftari la wapiga kura ambalo lilitumika kwenye uchaguzi wa mwaka 2019. TKU inasisitiza kwamba hakuna mwanachama ambaye ataruhusiwa kugombea nafasi ya uongozi, kupiga kura, au kupigiwa kura kama hatakuwa angalau amelipia ada ya uanachama kwa mwaka huu 2021”.
Kwa hivyo, pamoja na tangazo hili, ninawaomba wale ambao hawajalipa ada zao za uanachama wafanye hivyo mapema iwezekanavyo ili waweze kushiriki katika zoezi na jukumu hili muhimu kwa jumuiya yetu ya Waswahili wa duniani kote. Tunashukuru sana kwa ushirikiano mnaoendelea kutupatia. Wenu, Filipo Lubua Mkurugenzi wa CHAUKIDU
Uchaguzi wa Viongozi wa CHAUKIDU
1.0 UTANGULIZI 1.1. Kulingana na Katiba ya Chaukidu, ibara ya 6.3, viongozi wa chama pamoja na wajumbe wa Bodi wanapaswa kuchaguliwa na wanachama wenzao kila baada ya kipindi cha miaka miwili. Safu ya sasa ya viongozi wa juu wa chama cha CHAUKIDU pamoja na wajumbe wa Bodi ilichaguliwa mnamo mwezi Aprili 2019. Kwa maana hiyo, uchaguzi mwingine wa viongozi hauna budi kufanyika ifikapo Aprili 2021. 1.2. Kwa mujibu wa Katiba, ibara ya 6.4, kifungu cha 6.4.1. Tume ya Katiba na Uchaguzi (TKU) ndiyo imepewa mamlaka ya kuendesha shughuli ya uchaguzi wa viongozi wa chama. Na kwa mamlaka iliyonayo chini ya Katiba, TKU inapenda kutangaza nafasi za uongozi pamoja na ratiba ya uchaguzi wa viongozi wa chama kama ifutavyo hapa chini.2. NAFASI ZA UONGOZI
TKU inapenda kuwakaribisha wanachama kugombea nafasi zifuatazo za uongozi wa chama cha CHAUKIDU kwa kipindi cha miaka miwili ifuatayo (April 2021/April 2023).- Rais
- Makamu wa Rais
- Mkurugenzi
- Naibu Mkurugenzi Mweka Hazina (Mhazini)
- Katibu Mwenezi wa Chama
- Wajumbe sita (6) wa Bodi ya Wakurugenzi
3.0 RATIBA YA MCHAKATO WA UCHAGUZI Ifuatayo ni ratiba ya mchakato wa uchaguzi wa CHAUKIDU wa mwaka 2021.