Kwa wanachama wote wa CHAUKIDU Wakati tunajiandaa kukamilisha zoezi la upigaji kura na kuwapata viongozi wapya, Kamati ya Katiba na Uchaguzi (KKU) ingependa kutoa ufafanuzi ufuatao. Kwanza tunaomba kuwahakikishia wanachama wote wa CHAUKIDU kwamba KKU inatekeleza wajibu wake kwa weledi wa hali ya juu ikizingatia katiba ya chama, kanuni za uchaguzi na haki za kila mwanachama. Kwa mujibu wa Katiba ya CHAUKIDU, kila mwanachama anayo haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi iwe moja, mbili, tatu au zaidi. Wanachama wote walipewa nafasi hiyo. Wajibu wa mpiga kura ni kupima kila mgombea kwa nafasi zote alizoomba na kuamua kumpigia mgombea huyo kura yako kwa nafasi moja, mbili, tatu au zaidi alizoomba. Hata hivyo, kulingana na kanuni, endapo mgombea atakuwa ameshinda nafasi zaidi ya moja ya uongozi, basi KKU itampa ushindi kwa nafasi ya juu zaidi ya nyingine na kumwachia mgombea aliyefuata kwa wingi wa kura kuchukua ushindi kwa nafasi ya chini yake. Pia kulingana na kanuni, endapo mgombea atashinda nafasi za juu za uongozi (Rais, Makamu Rais, Mkurugenzi n.k) na pia ujumbe wa Bodi, basi jina lake litaondolewa kwenye ule ushindi wa Bodi na nafasi hiyo itachukuliwa na mgombea aliyefuata kwa wingi wa kura. Utaratibu huo tayari umeshatumika kwa washindi wa nafasi ya Mkurugenzi, Naibu Mkurugenzi na Mweka Hazina ambao walikuwa pia wameomba kugombea ujumbe wa Bodi. Kwa mujibu wa Katiba, viongozi hawa wa juu kwa nafasi zao wanaingia moja kwa moja kwenye Bodi. Mwisho tunapenda kuwahimiza wanachama wote washiriki kikamilifu katika mchakato wa upigaji kura wiki ijayo bila ya wasiwasi wowote. Kamati ya Katiba na Uchaguzi itahakikisha inalinda haki ya kila mgombea na kila mpiga kura. Kama tulivyoahidi, tumewatumia maelezo ya ziada ya baadhi ya wagombea ambao waliitikia wito wa kutuletea maelezo yao au wasifu wao pamoja na picha zao. Asanteni sana. Dr. Elias J. Magembe Kny. Kamati ya Katiba na Uchaguzi (KKU) – CHAUKIDU