Tangazo Muhimu Na. 003: Kuongezwa Muda
Kufuatia maamuzi ya kikao cha Bodi ya CHAUKIDU kilichofanyika tarehe 10 Machi 2019, Kamati ya Katiba na Uchaguzi (KKU) inatangaza rasmi kwamba muda wa kupokea mapendekezo ya wagombea umeongezwa na tarehe ya mwisho ya kupokea mapendekezo ya wagombea ni jumatano Machi 20, 2019. Uchaguzi huu utahusisha viongozi wafuatao: Rais, Makamu wa Rais, Mkurugenzi, Naibu Mkurugenzi, Mweka Hazina na Katibu Mwenezi wa Chama pia wajumbe sita wa Bodi wa kuchaguliwa. Kulingana na Katiba nafasi zingine kwenye Bodi zitajazwa na wajumbe wa kuteuliwa na Bodi mpya ya uongozi. Tuma mapendekezo yako haraka kabla ya muda uliotajwa hapo juu kwisha. Tunaomba utume mapendekezo yako moja kwa moja kwenye anuani ifuatayo ya Kamati ya Katiba na Uchaguzi ya CHAUKIDU: <kkuchaukidu@gmail.com>. Unaweza kujipendekeza au kupendekeza mwanachama mwingine kwa nafasi moja au zaidi ya moja. Ili uweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu (kuchagua au kuchaguliwa), ni muhimu kuhakikisha kwamba wewe ni mwanachama hai wa CHAUKIDU na uwe umelipa ada yako ya uanachama hadi mwaka huu wa 2019. Tafadhali hakikisha kwa kuangalia orodha ambayo imetumwa na Mkurugenzi. Kamati ya Katiba na Uchaguzi inawahakikishia kwamba itasimamia uchaguzi huu kwa UWAZI, HAKI NA UHURU ikizingatia kanuni na taratibu zilizoelezwa kwenye Katiba ya Chama. Utaratibu wa jinsi ya kupiga kura kwa njia ya kielektroniki utatolewa mara baada ya kumalizika kwa zoezi hili la sasa la kupokea mapendekezo ya wagombea. Asanteni sana, Dr. Elias J. Magembe Kny. Kamati ya Katiba na Uchaguzi – CHAUKIDU