Katiba

Katiba ya Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU)

 1. JINA LA CHAMA: Chama hiki kinaitwa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, na kwa hiyo kifupi chake ni CHAUKIDU.
 2. MAKAO MAKUU YA CHAMA: Makao makuu ya Chama Cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) yatakuwa katika mji na jimbo ambamo  rais wa chama hicho atakuwa anaishi  na kufanyia kazi. Makao makuu yanaweza kuhamishiwa katika sehemu nyingineyo kufuatia maamuzi ya uongozi wa bodi ya CHAUKIDU.
 3. MADHUMUNI YA CHAMA: Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni: Kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:

3.1.  Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.

3.2.  Kusambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na Kiswahili.

3.3.  Kuwajumuisha wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.

3.4.  Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.

3.5.  Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k.

 1. UANACHAMA: Wanachama watarajiwa ni pamoja na walimu, watafiti, wanafunzi, waandishi wa habari, wasanii, waandishi wa vitabu, wachapishaji, maafisa utalii, taasisi, n.k.

4.1.  Kujiunga na Chama: Bodi ya Uongozi itachunguza maombi yote ya uanachama na wanaokubaliwa watajiunga na chama kwa mujibu wa katiba hii. Kwa kuwa kujiunga kwa wanachama wapya hutegemea ulipaji wa  ada kwa mwaka, basi kiasi ambacho kitakuwa kikilipwa kila mwaka kitaamuliwa na Bodi ya Uongozi wa CHAUKIDU.

4.2.  Uanachama wa kulipia utakuwa wa aina mbili:

4.2.1.     Uanachama wa kibinafsi

4.2.2.     Uanachama wa kitaasisi

4.3.  Uanachama wa kutunukiwa: Uanachama huu unaweza kutolewa kwa mtu au taasisi yoyote kufuatia maamuzi ya Bodi ya CHAUKIDU kwa kuzingatia mchango wa mwanachama/taasisi hiyo katika kuchangia kuyafikia malengo ya chama.  

4.4.  Ada za Uanachama zitatofautiana kwa kuzingatia makundi yafuatayo:

4.4.1.     Mwanachama anayekaa/taasisi iliyoko:

4.4.1.1.         Afrika

4.4.1.2.         Kwingineko duniani

4.4.1.2.1.     Ada ya mwanachama asiye mwanafunzi

4.4.1.2.2.     Ada ya mwanachama mwanafunzi

4.5.  Haki na Majukumu ya Wanachama: Wanachama wote waliolipa ada wana haki zifuatazo:

4.5.1.     Haki za Wanachama:

          4.5.1.1.         Haki ya kuhudhuria mikutano ya chama

          4.5.1.2.         Haki ya kupiga kura katika uchaguzi wowote wa chama.

          4.5.1.3.         Haki ya kutoa maoni yao katika mikutano ya chama

         4.5.1.4.         Haki ya kupewa nakala moja ya kila kinachochapishwa na chama

         4.5.1.5.         Haki ya kugombea nafasi ya uongozi katika bodi ya chama au/na kamati za chama

4.5.2.     Majukumu  ya Wanachama.  Kila mwanachama ana majukumu yafuatayo:

         4.5.2.1.  Jukumu la kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazoendeleza  malengo ya chama

         4.5.2.2.  Jukumu la kuhudhuria mikutano ya chama

     4.5.2.3. Jukumu la kulipa ada ya uanachama pamoja na ada ya kila mwaka kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Uongozi bila kuchelewa.

      4.5.2.4.   Jukumu la kujiunga na kamati mbalimbali za chama

     4.5.2.5.   Jukumu la kujibu ujumbe wowote atakaopokea kutoka kwa chama ama wanachama kwa haraka inavyowezekana

    4.5.2.6.   Jukumu la kusasisha anuani yake katika kumbukumbu ya chama ili kiweze kuwasiliana naye.

     4.5.2.7.   Jukumu la kuyalinda na kuyatetea malengo ya CHAUKIDU.

4.6.  Kujiondoa Chamani kwa Hiari: Mwanachama yeyote anaweza kujiondoa kwa hiari kwa kuiandikia Bodi ya Uongozi tarehe ambayo angelipenda kujiondoa kwenye chama. Tarehe hiyo ikifika, mwanachama huyu atakuwa na haki ya kujiondoa kuwa mwanachama. Kuanzia tarehe anbayo atajibiwa haki na wajibu wa mwanachama huyo katika chama vinasimamishwa.  Mwanachama anayejiondoa mwenyewe chamani kwa hiari, hatarudishiwa sehemu yoyote ya ada alizolipa akiwa mwanachama.

4.7.  Kusimamishwa na Kuondolewa katika Chama: Mwanachama anaweza kuondolewa katika chama kwa muda au kwa jumla kulingana na jinsi Bodi ya Uongozi itakavyoamua.  Hali hii inaweza kutokea iwapo mwanachama huyo halipi ada ya mwaka, anafanya vitendo au anaonesha tabia ambazo  uongozi wa Bodi unaona ni hatari katika chama. Baada ya uongozi wa Bodi kutumia mamlaka iliyopewa na wanachama wote kupitisha azimio la kumsimamisha mwanachama, haki na majukumu ya mwanachama huyo vitasimamishwa mara moja.  Kama mwanachama amesimamishwa kwa muda, atarudishiwa haki na wajibu wake mara moja baada ya kumaliza kipindi alichokuwa amesimamishwa. Kipindi hicho lazima kiwe kimewekwa bayana katika azimio la Bodi ya Uongozi lililopitishwa ili kumsimamisha mwanachama huyo kwa muda.

 1. 5.     MIKUTANO YA WANACHAMA

5.1.  Mkutano wa kila mwaka: Bodi itawajibika kuitisha na kutangaza tarehe na mahali pa mkutano wa wanachama kila mwaka.

5.2.  Mikutano ya dharura: Bodi itakuwa na uwezo wa kutangaza mkutano wa dharura wakati wowote.  Ni lazima bodi imjulishe kila mwanachama kwa ujumbe ulioandikwa siku thelathini au zaidi kabla ya siku ya mkutano huo. 

5.3.  Idadi Inayohitajika: Theluthi mbili (2/3) za wanachama wenye haki ya kupiga kura zitatosha kujadili shughuli za chama na kupiga kura katika uchaguzi.  Ikiwa idadi hiyo haikufikiwa katika mkutano wa mwaka au mkutano maalum ulioitishwa na uongozi wa Bodi, uongozi huo umepewa mamlaka kuendesha mkutano wa shughuli kwa njia ya barua pepe. Ni wajibu wa mwanachama kujibu barua pepe aliyoipokea. Ni lazima theluthi mbili za wanachama au zaidi zipige kura katika uchaguzi kabla ya kura kusomwa.

5.4.  Utaratibu: Katika mkutano wo wote wa chama, Rais wa Chama atakuwa mwenyekiti wa mkutano.  Ikiwa Rais hayupo au hawezi kufanya kazi ya uenyekiti, wanabodi waliohudhuria watachagua mwenyekiti wa muda.  Ikiwa hakuna mwanabodi aliyehudhuria, wanachama waliohudhuria watachagua mwenyekiti wa muda.  Mkurugenzi wa chama atakuwa katibu wa mkutano.  Asipokuwepo au asipoweza kufanya ukatibu, mwenyekiti wa mkutano atachagua katibu wa muda.

5.5.  Uchaguzi:  Kwenye kila mkutano wa chama, kila mwanachama aliyelipa ada zake ana haki ya kupiga kura moja kuhusu kila suala linalojadiliwa. Mwanachama asipoweza kuhudhuria mkutano, ataweza kupiga kura bila kuwepo, ikiwa kura yake inamfikia Mkurugenzi wa Chama wiki mbili kabla ya mkutano. Zaidi ya asilimia hamsini za kura zinahitajiwa kushinda uchaguzi, kama kuna idadi (2/3) inayohitajika.

 1. Bodi ya Uongozi:

6.1.  Majukumu kwa Ujumla: Mali ya chama itasimamiwa na Bodi ya Uongozi na wanachama wote watakaokitumikia chama bila posho au malipo. Bodi ya Uongozi itaboresha mahusiano na vyama vingine ambavyo vitakuwa na malengo yenye mwelekeo kama wa CHAUKIDU.

6.2.  Idadi ya Wajumbe wa Bodi:  Idadi ya wawakilishi wa wanachama watakaochaguliwa moja kwa moja na wanachama wenzao kwa ajili ya kujiunga kwenye Bodi ya Uongozi itakuwa ni tisa. Pia kutakuwa na maafisa wafuatao: rais wa sasa wa chama, rais aliyemtangulia, mhariri mkuu wa machapisho, na mkurugenzi. Maafisa hawa watakuwa na haki kamili ya kupiga kura kama wajumbe wa Bodi ya Uongozi.

6.3.  Taratibu za Uchaguzi: Wajumbe wa Bodi ya Uongozi ambao si maafisa watachaguliwa na wanachama ili kuongoza kwa kipindi cha miaka miwili.  Mjumbe wa Bodi ambaye amemaliza muda wake anaweza kuchaguliwa tena baada ya kipindi cha mwaka mmoja. Kama kutakuwepo na nafasi wazi ya uongozi ambayo inatokana na sababu zozote zile inaweza kujazwa na wajumbe wa chama katika mkutano wa kwanza wa mwaka utakaofanyika baada ya nafasi hiyo kuachwa wazi. Kama si katika mkutano mkuu, Bodi inaweza kuitisha mkutano wa dharura kwa lengo la kujaza nafasi wazi.

6.4.  Mchakato wa Uchaguzi: Kutakuwepo na kamati ya uchaguzi yenye wajumbe wanne kama ifuatavyo: Wanabodi wawili watakaochaguliwa na Bodi kutokana na maofisa wa Bodi na wanachama wawili watakaochaguliwa na wanachama waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka. Kamati hii itatangaza nafasi za uongozi zilizo wazi na kuwataka wanachama wanaotaka kugombea watume maombi yao. Baadaye, kamati itapitia maombi hayo na kupendekeza majina ya wanachama watakaogombea nafasi za Bodi ya Uongozi. Kamati hii itapendekeza watu wawili kwa kila nafasi wazi inayojitokeza katika Bodi ya Uongozi.  Uchaguzi utafanyika kupitia njia ya barua pepe. Wanachama watatu watakaopata kura nyingi kuliko wengine watakuwa wamechaguliwa.

6.5.  Mkutano wa Mwaka: Bodi itaitisha mkutano wake kwa ajili ya kushughulikia maswala ya chama wakati na mahali itakapoamua mkutano huo ufanyikie. Uamuzi huo unaweza kufikiwa wakati wa mkutano au kwa kuwasiliana kupitia barua pepe.

6.6.  Mikutano ya Dharura: Mkutano wa dharura utaitishwa na bodi yenyewe kufuatia ombi la Rais wa chama au wajumbe watatu wa bodi hiyo.

6.7.  Taarifa ya mkutano wa dharura: Taarifa ya mkutano maalum ya Bodi lazima itolewe kwa kila mwanabodi kwa kumtumia taarifa hiyo katika anuani yake ya barua pepe aliyokuwa akiitumia kwa mara ya mwisho kabla ya taarifa hii.  Lazima taarifa hii itumwe siku kumi kabla ya siku ya mkutano.

6.8.  Idadi Inayohitajika: Ili kuweza kuendelea na mkutano wa Bodi lazima wajumbe watakaokuwa wamehudhuria wafikie angalau asilimia hamsini (50%) Ikitokea kuwa wajumbe hawafikii idadi inayotakikana, wajumbe walio wengi wa mkutano huo wataweza kupiga kura za kuuahirisha mkutano huo mpaka hapo baadaye idadi inayohitajika itakapokuwepo.

6.9.  Kujiuzulu: Mjumbe yeyote wa Bodi anayetaka kujiuzulu atatoa taarifa ya maandishi kwa Bodi siku thelathini kabla ya kujiuzulu.

6.10.   Kamati Mbalimbali: Rais atateua kamati mbalimbali kwa kadri zitakavyohitajika baada ya kuidhinishwa na Bodi ya Uongozi. Kila kamati itakuwa na wajibu wa kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa katiba hii. Wajumbe wa kamati hizo hawapaswi kuwa wanabodi ikiwa kazi za kamati hiyo inayoongelewa sio kazi nyeti ambazo lazima Bodi izishughulikie.

 1. Ofisi: Bodi ya Uongozi itachagua Rais ambaye ataiongoza kwa kipindi cha miaka miwili. Rais aliyemtangulia Rais wa sasa atakuwa mjumbe wa Bodi ya Uongozi katika muda unaofuata mwaka aliomaliza uongozi kama rais. Bodi ya Uongozi itateua Mkurugenzi wa Uongozi ili kuwa mjumbe wa Bodi kwa muda wa miaka miwili. Bodi ina mamlaka wakati wowote kuunda nafasi nyingine za uongozi na kuchagua viongozi wengine. Bodi inaruhusiwa kuteua maafisa kama ambavyo wataona inafaa ikiwa ni pamoja na kupanga posho kama zipo kwa kila aliyechaguliwa. Mkurugenzi wa Bodi na maofisa wengine walioteuliwa watashika madaraka kutokana na utashi ya Bodi ya Uongozi.

7.1.  Rais wa chama : Rais wa chama lazima asimamie mikutano yote ya chama na ya Bodi ya Uongozi. Anaweza pia kuitisha mikutano mbali ya mkutano mkuu wa wanachama wote. Rais atateua mwenyekiti wa mkutano wa mwaka ili kupanga mada na ajenda za mikutano ya chama. Rais lazima awe na uwezo wa kusimamia na kukagua masuala ya chama lakini anawajibika kwa Bodi ya Uongozi. Atakuwa na madaraka mengine na wajibu mwingine ambao haukuelezwa katika katiba hii kama ambavyo atakuwa amepewa wajibu au jukumu hilo na Bodi ya Uongozi.

7.2.  Mkurugenzi wa Chama: Mkurugenzi wa chama atafanya yafuatayo:

7.2.1.     Kutunza takwimu na nyaraka zote za chama;

7.2.2.     Kuwajulisha wanachama wapya kuwa uanachama wao umeidhinishwa;

7.2.3.     Kutunza nyaraka zikiwa na majina na anuani za wanachama;

7.2.4.     Kutunza mihtasari ya mikutano ya Bodi ya Uongozi;

7.2.5.     Kutunza pesa na nyaraka muhimu za chama;

7.2.6.     Kutoa risiti za ada na malipo mengine zinazolipwa katika chama;

7.2.7.     Kuziweka benki au kuziweka katika kampuni za uwekezaji pesa zilizopokelewa;

7.2.8.     Kuripoti matumizi na mapato katika Bodi ya Uongozi;

7.2.9.     Kuwaonyesha wajumbe wa Bodi ya Uongozi vitabu vya mahesabu;

7.2.10.  Kuhamasisha wanachama wapya;

7.2.11.  Kuchapisha au kuteua mtu wa kushughulikia gazeti la chama;

7.2.12.  Kushughulikia kuchangisha pesa kwa ajili ya chama;

7.2.13.  Kufanya shughuli nyingine ambazo Bodi ya Uongozi itaziidhinisha

7.3.  Kuondoshwa katika Uongozi: Kiongozi ye yote wa Bodi aliyechaguliwa au kuteuliwa anaweza kusimamishwa uongozi muda wowote na Bodi ya Uongozi ikiwa atashindwa kutekeleza wajibu kama kiongozi au kukiuka masharti ya uanachama.

7.4.  Kuteua Kiongozi wa Muda: Ikitokea kiongozi mmojawapo hayupo kwa sababu ambazo ni za msingi, Bodi inaweza kumteua mtu mwingine kushika nafasi hiyo kwa kipindi watakachoona kinafaa.

 1. Kuweka pesa benki, hundi (cheki), mikopo na mikataba:

8.1.  Kuweka Pesa benki: Pesa za chama lazima ziwekwe benki na/au katika kampuni za uwekezaji kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Uongozi. Bodi itaamua ni benki ipi inafaa kutumika kwa minajili hiyo.

8.2.  Hundi (cheki), n.k. Hundi zote na nyaraka za uthibitisho wa madeni ya chama lazima zisainiwe na ofisa au maofisa au wadhamini wa chama kama ambavyo Bodi ya Uongozi itaona inafaa. Ahadi ya pesa zilizoahidiwa na ambazo zinatakiwa kuwekwa katika akaunti ya chama zifanyike kulingana na Bodi itakavyoona inafaa.

8.3.  Mikopo: Hakuna mkopo au malipo ya awali yatakayofanywa kwa niaba ya chama na hakuna vithibitisho vya madeni vitakavyotolewa katika jina la chama, isipokuwa viwe vimeidhinishwa na Bodi ya Uongozi. Uthibitishaji wowote wa namna hiyo unaweza kuwa wa aina mbalimbali au matukio mahsusi kama vile ahadi, usalama wa mikopo au malipo ya awali yaliyopitishwa, na vitu vingine vikiwemo vitu binafsi vinavyoshikiliwa na chama.

8.4.  Mikataba: Hakuna mikataba itakayoidhinishwa kwa niaba ya chama isipokuwa ile tu iliyoainishwa na Bodi ya Uongozi kwa niaba ya chama.

8.5.  Kuhamisha fedha au Mali ya chama: Watu watatu, yaani Rais, Mkurugenzi, na mjumbe mmoja wa Bodi aliyeidhinishwa na Bodi ya Uongozi watakuwa na mamlaka ya kuidhinisha uhamishaji kama wa amana, pesa na mali nyingine kwa niaba ya chama.

 1. Mwaka wa Fedha:  Mwaka wa fedha wa chama utaanza tarehe 1 Oktoba na kumalizika tarehe 30 Septemba.
 2. Marekebisho ya Katiba:  Katiba itafanyiwa marekebisho katika mkutano ambao una theluthi mbili za wanachama wenye haki ya kupiga kura mradi tangazo la mkutano huo wa kushughulikia marekebisho ya katiba limetolewa kwa muda wa siku thelathini kabla ya mkutano huo.
 3. Kuidhinisha Katiba.  Katiba hii itaidhinishwa na kutumiwa badala ya katiba zo zote zilizoitangulia. Lazima katiba hii ikubaliwe na theluthi mbili za wanachama watakaohudhuria mkutano kulingana na mahali na tarehe iliyochaguliwa kwa ajili ya mkutano huo. Vilevile lazima tangazo la mkutano huo liwe limetolewa kulingana na muda uliobainishwa katika vifungu vya 5.2 na 10 hapo juu  ili wanachama wanaotakiwa kuhudhuria mkutano wa uamuzi kuhusu katiba mpya waweze kujiandaa kuhudhuria mkutano huo.
 4. Kutoa Mapato:  Mapato ya chama hayaruhusiwi kutolewa kwa ajili ya wanachama, maofisa au watu wengine binafsi, isipokuwa kuwalipa watu waliotoa huduma.