Wasilisha makala yako ikiwa katika MS Word kwa Wahariri kwa kutumia fomu maalumu ipatikanayo katika tovuti yetu: chaukidu.org/jarida
Jarida linachapishwa mara moja kwa mwaka mwezi wa Machi, waandishi wanaalikwa kutuma makala yao wakati wowote. Makala zitakazopokelewa kabla ya mwezi wa Oktoba ndizo tu zitakazokuwa na uhakika wa kuchapishwa kwenye toleo la jarida la mwezi Machi. Makala zitakazopokelewa kuanzia mwezi Oktoba zitachapishwa kwenye matoleo mengine yatakayofuata.
Hakuna ada yoyote kwa kuchapisha.
Ili kusaidia tahakiki fichishi, wasilisha makala yako bila kuweka jina lako, wala vidokezo vyovyote vya majina ya waandishi, taasisi wanakofanyia kazi, anuani-pepe zao, na nambari za ORCID kama wanazo. Makala ambazo hazitazingatia maelekezo haya, zitakataliwa na hazitafanyiwa tahakiki.
Waandishi wote ambao walichangia kwa kiasi kikubwa utafiti huo wanapaswa kuorodeshwa katika fomu maalumu ya kupokelea makala.
Jarida hili litachapisha makala zile tu ambazo hazijachapishwa na wala hazijawasilishwa kwa jarida jingine wakati linahakikiwa na wahariri wa jarida hili.
Lugha: Wasilisha makala yako kwa Kiswahili au Kiingereza. Ni muhimu sana uwapate wasomaji wengine ili upate jozi nyingine za macho ya kuhakikisha sarufi, tahajia na vituo vimetumika ipasavyo.
Font: Times New Roman 12 pt au inayofanana ya font hiyo.
Nafasi: Tumia 1.5 pt baina ya misitari.
Urefu wa makala: Kurasa zisizozidi 30.
Inashauriwa kugawanya maandishi katika sehemu zenye kichwa na nambari.
Ikisiri: Ikisiri isizidi maneno 200, iandikwe kwa Kiingereza NA Kiswahili. Ikisiri isiwe na tanbihi za chini ya ukurasa wala isiwe na marejeleo.
Chini ya ikisiri paandikwe istilahi muhimu za makala. Istilahi muhimu zisipungue tano.
Marejeleo: Tumia mtindo wa APA toleo la 7. Unaweza kupata maelezo kuhusu APA kwa kutumia kiungo Hiki Hapa.
Usitumie tanbihi isipokuwa tu pale ambapo kuna ulazima huo. aTanbihi, ikiwa itatumiwa iwe kama ifuatavyo: Tumia fonti ya 10 pt na tanbihi zitambulishwe kwa tarakimu 1, 2, 3, nk.
Nukuu: Data na maneno kutoka lugha nyingine yaandikwe kwa italiki. Tafsiri ya maneno ya kigeni ziwe katika alama za nukuu moja (`) na alama za nukuu mbili (“) zitatumika kuonesha nukuu za aina nyingine.
Nukuu: Kwa data na maneno yote yaliyoko katika lugha nyengine, tumia fonti ile ile, ila yaandikwe kwa italiki. Tafsiri ya maneno ya kigeni ziwe katika alama za nukuu moja (`) na alama za nukuu mbili (“) zitatumika kuonesha nukuu za aina nyingine.
UFAFANUZI
Makala zitakazokubaliwa zitakuwa zile:
Zinazofafanua utafiti jarabati unaopanua ufahamu wetu wa fasihi, isimu na utamaduni wa Kiswahili:
Zitajihusisha na data halisi, mbinu za kisayansi, vigezo vikuu
Utafiti unaothibitisha utafiti mwingine, au unaoonesha kasoro za utafiti mwingine katika nadharia, mbinu, matokeo au fasili ya matokeo.
Zinazotahakiki kazi za fasihi, utamaduni, na sanaa za Kiswahili
Riwaya, tamthiliya, ngano,
Mashairi, tenzi, nyimbo
Vibonzo, michoro, nk
Zinazotahakiki vitabu visivyo vya kifasihi.
Kuna vitabu vingine vingi ambayo si vya fasihi ambavyo vinahusu mambo mbalimbali ya lugha na utamaduni wa Kiswahili.
Zinazoendeleza mijadala na midahalo kuhusu mbinu za ufundishaji, na matini au vitabu vya kiada na ziada
Kote duniani walimu wa lugha wanabuni mbinu mpya za kuwashughulisha wanafunzi na kuwasaidia kupata stadi za lugha kwa haraka
Makala zaweza kulenga kuwashirikisha wadau au walimu katika mbinu hizo mpya
Zinazofanya uchunguzi au uchambuzi wa maendeleo na matumizi ya tenolojia katika nyuga zinazohusiana na lugha ya Kiswahili.
Teknolojia imeleta mbinu mpya katika ufundishaji
Zinazofanya uchambuzi wa kinadharia na kuongeza uelewa wetu wa mbinu za utafiti na mikabala ya uchunguzi katika nyuga mbalimbali za lugha ya Kiswahili na utamaduni wake.
Zinazochunguza na kujadili sera za lugha, na nafasi ya Kiswahili duniani
Zinazojadili kukua na kuenea kwa Kiswahili duniani.
Vigezo vya Tahikiki ya Makala
Kichwa/Anuani, ikisiri na makala kwa ujumla
Je, kichwa cha makala kinaendana na mada?
Je, ikisiri imezingatia vipengele vyake? Kwa mfano kama ni makala ya utafiti, mambo yafuatayo huzingatiwa:
Usuli
wali la utafiti
Mbinu za utafiti
Matokeo
Hitimisho
Je, ikisiri inawasilisha yaliyo katika makala?
Utangulizi
Je, utangulizi unafafanua na kutoa ramani ya makala?
Je, utangulizi unafafanua kwa muhtasari hoja au madai makuu ya makala?
Mada na mkabala
Je, mada inaeleweka na imewekwa katika muktadha wa kitaalamu?
Je, maswali ya utafiti yamenyooka?
Mkabala uliopendekezwa umeelezwa
Mapitio ya Maandiko
Je, maandiko yaliyopitiwa yanaendana na muda? Ni ya hivi karibuni au ya zamani?
Je, mapitio yamejikita zaidi katika vyanzo vizuri na vya kuaminika?
Waandishi wamechukua maandiko na kuyachunguza kwa kina?
Je, maandiko yaliyopitiwa yanahusiana kwa ukaribu na mada ya makala?
Umuhimu wa makala na malengo ya jarida
Makala inaendana na malengo ya jarida hili?
Jambo linalozungumziwa ni muhimu na waandishi wameonesha umuhimu huo
Utafiti unatoa mchango kwenye uwanja wa kisayansi unaohusika?
Usanifu wa utafiti
Utafiti unajaribu kujibu maswali gani?
Nadharia gani tete zimewekwa?
Mbinu za ukusanyaji wa data zinafaa kujibu maswali na kuthibitisha au kukanusha nadharia tete?
Sampuli zimeelezwa? Je, sampuli zinatosha au inawakilisha vema kwa utafiti huo
Uchambuzi:
Uwasilishaji wa matokeo
Mpangilio wa hoja, mifano na ufafanuzi unaridhisha?
Vielelezo, michoro, na mifano imewekwa kwa kufuata utaratibu na mpangilio unaokubalika na unaoleta mwanga?
Je, maelezo ya kufafanua na kuchambua vielelezo yanatolewa na yanaridhisha?
Kwa utafiti usio wa kisayansi, je, hoja zinatolewa ushahidi vipi?
Kujadili matokeo
Je, mjadala unalenga kujibu maswali yaliyotolewa mwanzoni?
Je, hoja zinafuata mantiki?
Mtindo
Je, lugha iliyotumika ni ya uwazi na yenye kufuata mtindo wa uwanja wa kitaaluma?
Je, makala imezingatia tahajia na kanuni za uwekaji vituo?
Je, sarufi iko sawa?
Je, makala inasomeka?
Orodha ya Marejeleo
Je, orodha ya marejeleo imezingatia kanuni za APA Toleo la 7?
MAKUBALIANO
Waandishi ambao wanachapisha katika jarida hili wanatoa ruhusa kwa jarida kuchapisha kwa mara ya kwanza kazi zao, na kazi hizo zina leseni chini ya Creative Commons Attribution Licence inayowaruhusu wengine kutumia kazi hizo kwa kumtambua mwandishi wa kazi na uchapishaji wa awali katika jarida hili.
TAARIFA YA MAADILI
Viwango vya maadili vya Jarida hili vimeainishwa kulingana na Miongozo Bora ya COPE kwa Wahariri wa Majarida. Miongozo hii inawahusu Waandishi, Wahariri, Wahakiki, na Mchapishaji.
Wajumbe wa Bodi ya Uhariri, Bodi ya Washauri, na wapitiaji wanafahamishwa juu ya Taarifa ya Maadili ya Uchapishaji na Udanganyifu wa Jarida kabla ya kuanza ushirikiano.
Miswada yote inayowasilishwa kwa jarida hili hupitiwa ili kuhakikisha kuwa inazingatia viwango vya maadili ya uchapishaji, pamoja na kutathmini uthabiti na thamani yake kisayansi. Mhariri Mkuu na Matbaa ya CHAUKIDU (Mchapishaji) wana wajibu wa kutekeleza sera hii.