CHAUKIDU secretariat@chaukidu.org

Blog Details

Chaukidu Nairobi 2016: Utangulizi

$0.00

Description

UTANGULIZI Leonard Muaka, Anne Jebet, David Kyeu na Beatrice Mkenda

Toleo hili ni matokeo ya ushirikiano mkubwa baina ya wasomi na wakereketwa wa Kiswahili duniani na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, ambao kwa pamoja wameweza kukusanya maoni na utafiti wa wataalamu wa Kiswahili ughaibuni na nyumbani Afrika katika toleo maalumu. Kwa hivyo, huu ni mkusanyiko wa makala yanayolenga kuchangia mjadala wa kukua na kusambaa kwa Kiswahili katika karne ya 21 huku mjadala wenyewe ukizingatia mchango wa Kiswahili katika nyanja mbalimbali za maisha ya wasemaji wa Kiswahili Afrika na ughaibuni. Toleo hili lina makala 18. Mengi yameandikwa na wanataaluma chipukizi, japo yapo baadhi yaliyoandikwa na wanataaluma wabobezi. Ni hatua ya mwanzo kabisa ya Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kuchangia kwenye hazina ya lugha ya Kiswahili kimawazo na kimkakati ili lugha ya Kiswahili iendelee kukua kiakademia na kijumuiya. Kupitia toleo hili, waandishi wanachangia kwa kuchanganua maswala muhimu ya kijamii katika karne ya ishirini na moja. Kwa jumla mada zilizoshughulikiwa ni pamoja na isimu kwa jumla, lugha na teknolojia, lugha katika miktadha ya kazi, na lugha kama chombo cha kuleta maendeleo ya jamii. Ni makala yanayowahamasisha wasomi na wakereketwa wa Kiswahili kuchangamkia lugha ya Kiswahili na kubadili mitazamo inayoidhalilisha lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za kiasili.

Releted Tags
    Share: